Posts

Showing posts from February, 2006

Mustakbali Mpya?

Miaka nenda, miaka rudi Tumekuwa tukitaradadi. Tumeelekea mbele, tumerudi nyuma. Kuzungukazunguka desturi yetu. Ramani waliyotupa tunayo mikononi Lakini yatuelekeza jangwani. Waliahidi kutufikisha mbuga za peponi. Leo twajikuta Jehanamu. Zi wapi hekaheka za madaraka na uhuru? Ndoto zetu zimekufa. Bendera zimecha kaa, zimeraruka. Tumeanguka, miguu imevunjika. Na bado twaimba nyimbo za kale. Eti twajivunia amani, uhuru na madaraka. Enzi za ukoloni zimepita, Lakini kujilisha, kujivisha tumeshindwa. Eti amani, uhuru na madaraka? Ndiyo. Amani, uhuru na madaraka; Madaraka ya vibaraka; Wanavijiji mafukara wa “Global Village”. Watoto wa bara wameamka. Urithi wetu hawautaki, mienendo yetu wanaikana. Lakini mwana wa nyoka ni nyoka. Wataujenga upya uafrika? This poem is licensed under a Creative Commons Attribution-Noncommercial 3.0 Unported License . Please feel free to use my writing for non-commercial purposes and do credit my name, Rose